Rozari hai ilipata idhini ya kanisa tangu mwanzo kabisa. Askofu mkuu wa Lions, kule ilikoanzia,  alitoa idhini yake mara moja na kuikamilisha ibada hii jimboni mwake.

Mnamo mwaka 1832 Kanisa liliwachagua wakurugenzi wawili waongoze ushirika huu wa Rozari hai. Huu ni ushahidi kuwa kanisa lilikubali na kuruhusu ushirika huu uendelee, mpaka ikaona umuhimu wa kuchagua wakurugenzi waongoze.

Papa Gregori XVI ndiye aliyetoa idhini rasmi kuruhusu ushirika huu wa Rozari hai. Na yeye aliyemchagua Filomena awe somo na mlinzi wa ushirika huu wa Rozari hai. Papa huyu alitoa rehema nyingi sana kwa wenye kusali Rozari hai (tazama rehema: sura ya nane kitabu cha Faraja ya Uponyaji wa Moyo wa Maria). Tangazo rasmi la Papa Gregori XVI kuruhusu Rozari Hai tarehe 27/1/1832. Nalo ni kama lifuatalo:
“ Katika uchungu mkubwa, matatizo na shida za siku hizi, kitulizo chetu ni ibada hii kwa Bikira Maria ijulikanayo kwa jina la ROZARI HAI. Tunaishi chini ya tumaini kubwa la msaada wa Mungu. Faida kubwa ya ibada hii ni ule urahi wa kuishi, na vile inavyotufanya tumgeukie Mungu kwa njia ya Bikira Maria. Umoja uliopo baina ya watu wengi walioungana katika kusali, hufanya sauti yao iwe kubwa na kumfanya Mungu atuhurumie.

“Kwa ajili hii hatusiti kuwahubiria juu ya zoezi hili la Rozari hai kwa uwezo wetu wa kipapa, na tutatoa rehemu nyingi, huku tukikumbuka siku zote faida kubwa za ushirikiano tunapomwomba Bikira Maria kwa kusali Rozari. Mapadri wetu popote wamejitoa kukaribisha uanzilishaji wa Rozari hai, na wengi wao wameipendekeza Majimboni mwao, kama ibada ya pili baada ya Sakramenti, na hivyo kuvuta Neema na Baraka kwa wote”.
Maaskofu  wengi sana wameipokea ibada hii ya Rozari hai Majimboni mwao, na kuithamini  kama ni chombo bora sana kwa kuboresha maisha ya Wakristu wao.